HISTORIA- SEPTEMBA 9, 1990: KIFO CHA DIKTETA SAMUEL DOE WA LIBERIA.

samuel-kanyon-doe-copySamuel Kanyon Doe alizaliwa May 6, 1951 jijini Tuzon, nchini Liberia…
Alfajiri ya Aprili 12, 1980, kikundi kidogo cha wanajeshi 17 kilijipenyeza ndani ya makazi ya Rais jijini Monrovia… Ikulu walimkuta Rais William Tolbert bado amelala… Wakamuua… Aliyeongoza kikundi hicho alikuwa askari kijana na wa cheo cha chini, Sajenti Samuel Doe…
Na inasemwa kuwa Doe alipoingia Ikulu na wenzake, alidhani watakwenda kumlalamikia Rais juu ya mishahara midogo ya askari wa vyeo vya chini… Lakini jinsi walivyoikuta Ikulu ikiwa nyepesi vile, ndivyo mipango ilipobadilika na kuamua kumuua Rais mwenyewe na kuchukua madaraka…
Samuel Doe alikuwa askari ambaye hata madarasa manne ya shule ya msingi hakuyamaliza… Alitoka kabila dogo la waishio misituni, kabila la Krahn… Ni watu wa kabila kama lake, masikini na ambao ndio waliotoka vijijini na kukimbilia jijini Monrovia kutafuta vibarua na pesa… Kwa wenye bahati, kama Samuel Doe, walionekana mitaani na kuitwa kujiunga na Jeshi…
Na kama ilivyokuwa kwa Idi Amin, Urais ulimdondokea tu Samuel Doe, kama vile mtu aliyeshinda bahati nasibu…
Ujio wa Samuel Doe uliwafaya WaLiberia waamini kuwepo kwa mabadiliko… Kuondokana na utawala wa kifisadi na kirasimu wa William Tolbert…
Samuel Doe akajitangaza kuwa Rais, April 12, 1980… Haraka sana akawatwanga risasi mawaziri wote wa Tollbert… Ni kwenye pwani ya bahari huku wananchi wakitazama kama mechi ya mpira…
Sajenti Samuel Doe akatawala kwa kipindi cha miaka kumi… Nchi ikawa kama imesimama….
Watu wa kabila la Samuel Doe waliogopewa na makabila mengine… Waliweza kufanya lolote lile na hakuna aliyewagusa… Waliua na waliwatisha wengine… Wengi wasio wa kabila la Rais Doe, waliishi kwa hofu kubwa…
Na kile ambacho kila mtu asiye wa kabila la Doe, alikuwa anakisubiri, ni kushuhudia mwisho wa Sajenti Samuel Doe…
Na hapa akatokea Charles Taylor… Huyu alikuwa rafiki wa zamani wa Sajenti Samuel Doe…
Lakini, urafiki wao ulikufa pale Samuel Doe alipodai kuwa Charles Taylor alimtapeli dola milioni moja… Kisha Taylor akatorokea Marekani… Huko akaanza kufanya biashara kwa mtaji wa fedha alizomtapeli Sajenti Samuel Doe…

Charles Taylor
Charles Taylor

Charles Taylor naye akaishia gerezani nchini Marekani kwa mashtaka ya utapeli… Lakini akatoroka jela na kukimbilia Ivory Coast… Na akiwa Ivory Coast, Charles Taylor akaanza kujipanga kwenda kuuangusha utawala wa Sajenti Samuel Doe… Charles Taylor akiwa Ivory Coast, alikiandaa kikosi cha wapiganaji 60… Kikosi kilikuwa tayari kwa kuingia Monrovia kumwondoa Samuel Doe madarakani…
Ilikuwa ni mwaka 1989… Wakati huo, wajuzi wa masuala ya kijeshi waliamini kabisa, kuwa Sajenti Samuel Doe angeweza, kirahisi kabisa, kumteketeza kijeshi Charles Taylor na kikosi chake cha watu 60… Sajenti Samuel Doe angeweza kufanya hivyo hata kabla Charles Taylor hajavikaribia viunga vya Monrovia…
Badala yake, ‘’Master Sergeant’’ Samuel Doe, aliwatuma mstari wa mbele, wanajeshi kutoka kabila lake la Krahn… Ni wanajeshi wa kuokoteza ambao wengine hawakuwa hata na viatu… Wanajeshi wale wa Samuel Doe, njiani wakitokea mji mkuu Monrovia wakielekea uwanja wa mapambano, wakaanza kufanya wizi wa ngawira, kuiba mali za watu…
Habari za askari ‘’vibaka’’ wa Samuel Doe zikasambaa haraka kwenye vijiji vya msituni…
Huko watu wakajitolea kujiunga na vikosi vya Charles Taylor kukabiliana na askari wa Samuel Doe…
Jeshi la Taylor likakua kwa haraka… Baada ya miezi sita tu, likaingia kwenye viunga vya mji mkuu wa Liberia, Monrovia, June 1990…
Ndipo hapo kwenye kambi ya Charles Taylor ugomvi ukazuka… Nani atakuwa Rais???… Nani atakuwa na mamlaka ya hazina kuu???… Ni ugomvi uliowatenganisha Charles Taylor na Prince Johnson aliyeamua kuachana na Taylor na yeye kuanzisha kikosi chake…
Wote wawili walikuwa na tamaa ya Ikulu. Vita sasa ikawa ya vikosi vitatu kugombania kuingia Ikulu ya Monrovia: Kikosi cha Sajenti Samuel Doe kinachojihami, kikosi cha Charles Taylor na kikosi cha Prince Johnson… Wote wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe kugombania Ikulu ya Monrovia…
Mitaa ya Monrovia wakaonekana askari wa makundi tofauti wakipigana. Hata watoto waliingizwa kwenye vita vile vya kiwendawazimu…
Hatimaye, mwishoni mwa mwezi August 1990, vikosi kutoka nje viliingilia mgogoro ule… Ni vikosi vya Nigeria chini ya mwavuli wa ECOMOG, ni umoja wa mataifa ya Afrika Magharibi… Ecomog walikuwa na jeshi lilioongozwa na kamanda kutoka Nigeria… Jeshi hilo lilifika Monrovia na meli kubwa ya kijeshi…
Jumapili Septemba 9, 1990, Rais Samuel Doe aliposikia habari za ujio wa ECOMOG, akafanya kosa kubwa la kuamua kutoka Ikulu na kwenda mwenyewe bandarini kuonana na kamanda wa vikosi hivyo vya majeshi ya Nigeria… Samuel Doe hakuwa na msafara mkubwa… Aliwachukua walinzi wake na kuingia kwenye Mercedes Benz kuelekea bandarini…
samuel-kanyon-doe1Masikini, Rais wa nchi akajikuta anapita kwenye mji wenye miba… Akafika bandarini na hapo Prince Johnson alikuwa amewapanga askari wake kumshughulikia Samuel Doe… Zikapigwa risasi na walinzi wote wa Samuel Doe wakapoteza maisha… Samuel Doe mwenyewe risasi ilimpata mguuni na hakuweza kukimbia, akakamatwa…
Akafungwa kitambaa usoni na akapelekwa kwenye kuteswa… Prince Johnson akahakikisha mateso yale yanarekodiwa kwa kamera za filamu… Kwenye filamu hiyo, Prince Johnson anaonekana akipungiwa upepo na mwanadada huku akinywa bia na kumwangalia rafiki yake wa zamani, Samuel Doe akiteswa… Muda mwingi Prince Johnson alikuwa akimtaka Samuel Doe aseme zilipo fedha kwenye hazina…
Kuna wakati alisikika Samuel Doe akimwita rafiki yake wa zamani kwa jina alilozoea kumwita: “Prince, waambie walegeze kamba walizonifunga, nitasema kila kitu, walegeze hizo kamba kwanza!”…
Ukweli, kamba walizomfunga kwenye miguu na mikono zilikaza sana na kumletea maumivu makali… Waliendelea kumpiga huku wakimtaka ataje ilipo hazina. Walimtaka ataje akaunti yake ya benki…
Ndivyo ilivyokuwa barani kwetu Afrika, na labda mpaka leo… Rais dikteta anapopinduliwa, kikubwa kinachotafutwa ni namba ya akaunti ya benki alikoficha fedha… Mara nyingi ni kwenye benki za nje… Ndio, inahusu hazina ya nchi…
“Mkateni sikio kama hataki kusema!” Alisikika Prince Johnson akitamka kwa hasira…
Askari wale wakamtupa Samuel Doe sakafuni, wakamkata sikio moja…
“Mkateni sikio lingine!”, alisikika tena Prince Johnson akitamka…
Baada ya hapo, Rais Doe aliuawa kikatili Jumapili hiyo jioni, Septemba 9, 1990 baada ya kukatwa masikio yake, sehemu zake za siri na baadhi ya vidole vya miguu na mikono na hatimae mwili wake ulitembezwa mitaa mbalimbali ya jiji la Monrovia…
Huo ndio ulikuwa mwisho wa Dikteta Samuel Kanyon Doe wa Liberia….